Wananchi wa Mvomero wataka mgogoro wa ardhi katika bonde la Mgongola utatuliwe

Wananchi wa wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro wameomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi, kumaliza mgogoro wa miaka mingi wa ardhi katika bonde la mpunga la Mgongola.

Wameomba umalizwe haraka na suluhu la kudumu ipatikane ili kukomesha matukio ya mauaji ya wakulima na wafugaji wa vijiji mbalimbali vya Kata ya Hembeti wilayani humo.

Ombi hilo lilitolewa na baadhi ya wakazi wa vijiji cha Dakawa, Hembeti na Mkindo, kwa nyakati tofauti. Walidai wanasikitishwa kuona kesi namba 127/2005 iliyofunguliwa mwaka 2005, haijamalizika hadi leo.

Kutoisha kwa kesi hiyo, kumechochea mgogoro kati ya wananchi vijiji vinavyozunguka Bonde la Mgongola na jamii ya wafugaji wa kijiji cha Kambala wanaodai sehemu kubwa ya bonde ni mali yao.

“Ni miaka mingi sasa imepita, hakuna ufumbuzi wa kudumu...imekuwa ni zimamoto kutuliza mgogoro unapoibuka na kusababisha mauaji,” alisema mmoja wa wanakijiji ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Alisema, kila yanapotokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji, polisi hufanya kazi ya kutuliza kwa njia ya kufyatua mabomu ya machozi ufumbuzi ambao siyo endelevu.

Novemba mwaka jana yalijitokeza mapingano ya siku tatu kuanzia Novemba 4 saa 10 jioni hadi Novemba 6, katika vijiji vya Kata ya Hembeti, wilayani Mvomero na yalisababisha vifo vya watu sita na kujeruhi watu 36.

Mapigano hayo yaliyotokea kati ya kikundi cha Mwano kilichokuwa kikiungwa mkono na wakulima na wafugaji wa Kimasai. Chanzo cha mapigano hayo ni baada ya ng’ombe 300 wa mfugaji Semwako Matunda kutoka kitongoji cha Mpapa Kata ya Hembeti kuingia kwenye mashamba ya wakulima wanne na kuharibu mazao mbalimbali.

Novemba 6, 2014 yalitokea mapigano mengine eneo la Kitongoji cha Mpapa kijiji cha Kigulukilo, kati ya kikundi cha Mwano na wafugaji na kusababaisha vifo vya watu watano na majeruhi 28.

Februari mwaka huu, mkulima Abdallah Shomari (27), mkazi wa Kingolwira aliuawa na kundi la wamasai katika bonde la mpunga la Mgongola, ambapo watuhumiwa watano walikamatwa na wamefikishwa mahakamani.

Tukio lingine la mauaji lilikuwa Aprili 24, mwaka huu, ambapo watu wawili walikufa kutokana na mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika eneo Kijiji cha Mkindo wilayani Mvomero.

Waliokufa kutokana na mapigano hayo ni Kipasisi Kashu (19), mfugaji na mkazi wa kijiji cha wafugaji cha Kambala na Shukuru Juma (23) ambaye ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kigugu Kata ya Hembeti, wilayani humo.

Chanzo za mapigano hayo ni uhasama kati ya wakulima na wafugaji. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo kiini cha mapingano hayo ni ng’ombe 306 wa wafugaji kula mazao katika shamba la mkulima, Ignas Ramadhani, Aprili 23, mwaka huu.

Polisi ilirejesha hali ya utulivu katika eneo la mapigano kwa kufyatua mabomu kadhaa ya machozi na risasi hewani. Kamanda Paul alisema ulinzi umeimarishwa katika vijiji vinavyopakana na bonde hilo la Mgongola, kuzuia mapigano kujitokeza tena.
Share on Google Plus
    Blogger Comment
    Facebook Comment

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment