MH PAUL MAKONDA TUNAOMBA MTUTATULIE KERO YA GEREJI BUBU KINONDONI STUDIOKwenu timu ya Keroyako.com,

Mimi ni mkazi wa Kinodoni Studio na katika eneo letu tumekuwa tukisumbuliwa na kero ya gereji bubu kwa muda mrefu sana (zaidi ya miaka 10).

Kwa kweli tatizo hili sugu linatusumbua sana wakazi wa mtaa wetu (Luichi Street), ni mtaa kabla ya barabara ya Mwinjuma (barabara ya kwenda Mwananyamala), upande wa kushoto ukitokea Magomeni.

Gereji hii ilivamia mtaani baada ya ujenzi wa kwanza wa barabara ya Morocco (kwa sasa Kawawa) ilipopanuliwa na kujengwa lane 2 kila upande.  Upanuzi huu ulipelekea baadhi ya nyumba kuvunjwa na mojawapo ya nyumba hizo zilizovunjwa ilikuwa imepangisha hao watu wa gereji kufanya biashara zao.  Kabla ya upanuzi shughuli za gereji hiyo zilikuwa zikifanyika kwa upande wa barabara kuu (Kawawa Road).  Baada ya upanuzi hakukuwa na nafasi ya kufanya shughuli zao hivyo pole pole walianza kujisogeza upande wa mtaa wa Luichi na kuendelea na shughuli zao za kutengeneza magari.

Kero kubwa zinazotukabili kutokana na kuwepo kwa gereji hiyo ni pamoja na:-

1.  Uchafuzi wa mazingira (kutupa vipuri chakavu hovyo pamoja na kumwaga oil chafu hovyo).

2.  Kuziba mifereji ya maji machafu, wamekuwa wakitumia mifereji ya kupeleka maji machafu kwa kumwaga oil chafu pamoja na filter na vipuri vingine vidogo vidogo ambavyo vinaweza kupenya kwenye mashimo ya maji machafu.  Uchafuzi huu umesababisha mafuriko kwa nyumba za mtaa huo kiasi kwamba maji yanaingia ndani ya nyumba jambo ambalo halikuwa la kawaida kabla ya uwepo wa gereji hiyo.

3. Kuziba mageti ya wakazi wa maeneo hayo.  Mafundi wa gereji hiyo hawana ustaarabu kabisa kiasi kwamba wakipata wateja hupaki magari yao popote tu ili mradi kuna nafasi ya kutosha kupaki gari.  Kitendo hicho kimesababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wenye magari mara wanapotaka kutoka ndani au pale wanaporejea nyumbani na wanahitaji kuingiza ndani magari yao.  Hali hii imepelekea magomvi ya hapa na pale kati ya mafundi na wenye nyumba na hali hiyo bado inaendelea kama inavyoonekana katika picha zilizoambatanishwa na mail hii.

Wakazi wa eneo hili wamepeleka kero hii kwa uongozi wa Wilaya ya Kinaondoni miaka ya nyuma lakini suluhu haikupatikana kabisa.  Uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mwinjuma pia unalifahamu suala hili lakini nao pia hawakuweza kutoa msaada wowote. 

Kwa kuwa hali hii inawatia unyonge sana wakazi wa mtaa (ambao ndiyo walipa kodi za Serikali na pia wapiga kura wa viongozi mbalimbali) kuona kero zao zinapuuziwa na hawa watu ambao ni wavamizi wanaendelea kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya nyumba zao na kuendelea kuchafua mazingira bila kuchukuliwa hatua stahili.

Tunaomba timu ya Kero Yako itusaidie kumpelekea muhusika ambaye anaweza kututatulia tatizo hili ili wananchi waweze kuishi katika mazingira safi.
Share on Google Plus
    Blogger Comment
    Facebook Comment

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment